Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah al-Udhma Makarim Shirazi katika ujumbe wake, huku akisisitiza umuhimu wa ushiriki mkubwa wa wananchi katika hafla ya kuaga na mazishi ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi, amesema: Vita havijaisha; kwa hiyo, aina yoyote ya kueneza kukata tamaa, kulegeza ari, kuonesha kwamba hakuna njia ya kutoka, na kudhoofisha morali ya wananchi, viongozi na vikosi vya ulinzi, ni kwenda sambamba na matakwa ya adui na ni kinyume na maslahi ya nchi na Umma wa Kiislamu.
Kiongozi huyo pia alisisitiza ulazima wa kudai kisasi kwa ajili ya Imam Shahidi na katika muktadha huo akasema: Wauaji na wahusika wa jinai hii kubwa, ambao mikono yao imelowa damu ya shahidi huyo mpendwa, makamanda, viongozi, wananchi wasio na ulinzi na watoto walio dhulumiwa, hawatasalimika na adhabu ya Mwenyezi Mungu wala hukumu ya haki. Umma wa Kiislamu nao, ndani ya mipaka ya Sheria, utaendelea kutekeleza wajibu wake wa kudai kisasi kwa ajili ya mashahidi hawa.
Kushikamana na Wilayatul Faqih ni moja ya mihimili mingine muhimu ya ujumbe wa Ayatullah Makarim Shirazi. Kuhusu jambo hili amesema kwamba: Mapinduzi ya Kiislamu yamesimama juu ya msingi wa kanuni tukufu ya Wilayatul Faqih, na kwa baraka za kanuni hiyo ndiyo yamefanikiwa kuvuka njia ngumu na njama nyingi za maadui. Wilayatul Faqih katika mfumo wa Kiislamu ndiyo mhimili wa umoja, mlinzi wa maslahi ya Umma na nguzo imara ya mfumo wa Kiislamu; na kushikamana nayo ni wajibu wa kila mmoja na ndiyo njia ya kuilinda Uislamu na nchi.
Maandishi kamili ya ujumbe wa Ayatullah Makarim Shirazi ni kama ifuatavyo:
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu
﴿إِنَّا لِلَّهِ وَإِنَّا إِلَیْهِ رَاجِعُونَ﴾
Sambamba na hafla ya kuaga na mazishi ya mwili mtukufu wa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi, majonzi makubwa ya kumpoteza mwanajihadi huyo mwenye hekima yamehuishwa tena. Bila shaka, ushiriki mkubwa wa wananchi katika hafla hii utakuwa ni dhihirisho la nguvu na uaminifu kwa malengo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu, ishara ya uthabiti wa taifa kubwa la Iran na Umma wa Kiislamu, pamoja na mwendelezo wa njia yenye nuru ya mashahidi.
Katika mazingira haya, kuzingatia mambo kadhaa ni muhimu:
Kwanza: Haifai kudhani kwamba vita hivi vimekwisha; bali mapambano dhidi ya kambi ya ubeberu bado yanaendelea. Kwa hiyo, aina yoyote ya kueneza kukata tamaa, kulegeza ari, kuonesha kwamba hakuna njia ya kutoka, na kudhoofisha morali ya wananchi, viongozi na vikosi vya ulinzi, ni kwenda sambamba na matakwa ya adui na ni kinyume na maslahi ya nchi na Umma wa Kiislamu. Bila shaka, matumaini na uthabiti kamwe havimaanishi kupuuza uhalisia wa uwanja wa mapambano; bali subira na kusimama imara ni miongoni mwa sababu muhimu zaidi za kupata ushindi katika mitihani ya Mwenyezi Mungu.
Pili: Wauaji na wahusika wa jinai hii kubwa, ambao mikono yao imelowa damu ya shahidi huyo mpendwa, makamanda, viongozi, wananchi wasio na ulinzi na watoto madhulumu, hawatasalimika na adhabu ya Mwenyezi Mungu wala hukumu ya haki. Damu hizi safi hazitasahaulika kamwe, na Umma wa Kiislamu, ndani ya mipaka ya kisheria, utaendelea kutekeleza wajibu wake wa kudai kisasi kwa ajili ya mashahidi hawa.
Tatu: Viongozi, vikosi vya ulinzi na wote wanaofanya maamuzi wanapaswa, kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu, kuamini ahadi Zake, kutumia uwezo wote wa nchi na kutegemea imani, subira na uthabiti wa wananchi, kwa busara, nguvu na umakini, iwe katika medani ya kijeshi, diplomasia au nyanja nyinginezo, kusimama kidete mbele ya adui. Kwa sababu uzoefu umeonesha kwamba aina yoyote ya kurudi nyuma mbele ya adui mvamizi humfanya azidi kuwa jasiri katika kuendeleza uvamizi na tamaa zake.
Nne: Mapinduzi ya Kiislamu yamesimama juu ya msingi wa kanuni tukufu ya Wilayatul Faqih, na kwa baraka za kanuni hiyo yamevuka njia ngumu na njama nyingi za maadui. Wilayatul Faqih katika mfumo wa Kiislamu ndiyo mhimili wa umoja, mlinzi wa maslahi ya Umma na nguzo imara ya mfumo; na kushikamana nayo ni wajibu wa wote na sababu ya kuulinda Uislamu na nchi.
Tano: Leo kuliko wakati mwingine wowote, kulinda umoja na mshikamano wa kitaifa ni jambo lisiloweza kupingika. Hairuhusiwi tofauti za maoni, hata kama zimetokana na nia njema, kuwa sababu ya kuibua mifarakano na kudhoofisha safu ya ndani ya nchi. Wakati huo huo, viongozi waheshimiwa wanapaswa kwa juhudi zaidi kujitahidi kutatua matatizo ya wananchi na kuwahudumia kwa uaminifu.
Kwa mara nyingine tena, ninatoa mkono wa pole kwa tukio la kuumiza la shahidi mpendwa pamoja na mashahidi wengine wa vita hivi vya kulazimishwa, kwa Mtukufu Imam wa Zama (aj), Kiongozi Mtukufu wa Mapinduzi, familia zenye heshima za mashahidi, taifa tukufu la Iran na Waislamu wote duniani. Ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awape daraja za juu, na ninatumaini kwamba, chini ya kivuli cha usimamizi wa Imam wa Zama (aj), utukufu na ushindi wa Uislamu na Waislamu pamoja na kuondolewa shari za maadui vitapatikana haraka iwezekanavyo.
Wassalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh
Qom
Nasir Makarim Shirazi
Maoni yako